Rugemalira amewasilisha hoja ya kufutiwa kesi ya uhujumu uchumi

Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mfanyabiashara James Rugemalira utawasilisha majibu ya hoja za mfanyabiashara huyo anayetaka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imuondoe katika kesi ya uhujumu uchumi.

Rugemalira amewasilisha hoja hizo leo Februari 27, 2020 wakati shauri hilo lilipoitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.

Mahakama hiyo imepokea hoja hizo na upande wa mashtaka wamesema kuwa watawasilisha majibu yao kwa njia ya maandishi kabla ya Machi 12, 2020.

Rugemalira amefikia hatua hiyo, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kueleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Simon amesema mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi kuwa kesi iliitwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba bado wanaendelea na upelelezi.

Baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, John Chuma anayemwakilisha Rugemalira alisema mahakamani hapo kuwa mteja wake aliwasilisha hoja ya pingamizi la awali ambayo mpaka sasa hawajapata majibu yoyote.

Akijibu hoja hiyo Simon alikiri kupokea nyaraka mbili kutoka upande wa utetezi moja ikiwa inamhusu Rugemarila lakini alitaka kujua kama nyaraka hizo zipo kwenye rekodi ya mahakama.

Hakimu Shahidi amesema ameziona nyaraka hizo na zipo kwenye rekodi ya mahakama.

Kutokana na hali hiyo, Simon aliieleza mahakama kuwa watatoa majibu kwa mdomo mahakamani hapo baada ya upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao kwa maandishi na wako tayari kujibu muda wowote ikiwa mahakama itaruhusu.

"Hata leo kama mahakama inaturuhusu tunaweza kutoa majibu dhidi ya hoja yaliyowasilishwa na mshtakiwa mahakamani hapa," amesema Simon.

Awali Rugemalira alisema mahakamani kuwa aliandika barua kwa Kamishna wa TRA kupitia mjumbe wa Takukuru aliyetembelea gerezani akielezea jinsi Benki ya Standard Chartered Hong Kong inavyokwepa kodi huku akieleza kuwa wanaostahili kujumuishwa kwenye kesi ni benki hiyo na si yeye.

Rugemalira amesema pia aliandika notisi kwa taasisi tisa ikiwemo Usalama wa Taifa (TISS) akitaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) awasilishe hati ya kuachiwa kwake na asipofanya hivyo yeye atawasilisha hoja ya kuiomba mahakama imuondoe katika kesi hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Shaidi aliwaagiza upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao kwa maandishi Machi 2, 2020 na upande wa mashtaka wamesema watatoa majibu kabla ya Machi 12, 2020.

Pia, Hakimu Shaidi amesema endapo upande wa utetezi watakuwa na hoja za nyongeza baada ya kupata majibu wapaswa kuyawasilisha Machi 14, 2020.

Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 12, 2020 itakapotajwa.