Na Ahmad Mmow, Lindi.
Chama cha ACT-Wazalendo jimbo la Lindi mjini leo kimeonesha kitashiriki uchaguzi mkuu kupitia nafasi ya ubunge. Baada ya aliyepitishwa na chama hicho awe mgombea wake katika jimbo la Lindi mjini, Isihaka Mchinjita kuchukua fomu ya serikali kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa manispaa ya Lindi.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi za halmashauri ya manispaa ya Lindi baada ya kuchukua fomu hizo, alisema ameamua kugombea ubunge ili arejeshe nguvu za upinzani katika jimbo hilo iwapo atakuwa mbunge.
¥ Mchinjita ambae amewahi kugombea nafasi hiyo katika jimbo la Mtama kupitia Chama Cha Wananchi-CUF mwaka 2015 alisema nijambo lililowazi kwamba wananchi wameondokewa imani na utendaji wa wawakilishi wao. Hasa katika nafasi ya ubunge, hali iliyosababisha wapoteza jimbo hilo.
Alisema kufuatia hali hiyo ameona kunahaja ya kuwa na mgombea makini anayetoka katika chama makini ambaye atakuwa mwakilishi sahihi wa wananchi wa jimbo hilo ambao wanamtaka mwakilishi ambaye licha ya kuwasemea lakini atakuwa sehemu ya wao wakati wa shida na raha.
Aidha Mchinjita alisema Chama Cha Wananchi-CUF kilikuwa na nguvu katika mikoa ya Lindi na Mtwara kabla ya chama hicho kukumbwa na mgogoro wa uongozi. Hatahivyo kutokana na mgogoro ulioibuka baada ya kumalizika uchaguzi wa mwaka 2015 kimekosa nguvu.
'' Ulisababisha kutumia muda mwingi kutafuta suluhisho, nakujikuta tunashindwa kujenga chama. Hali iliyosababisha baadhi yetu kujiondoa nakujiunga na vyama vingine. Kwangu mimi chama mbadala kinachoweza kurejesha nguvu za upinzani na imani ya wananchi ni ACT-Wazalendo,'' alisema Mchinjita.
Mtia nia huyo aliweka wazi kwamba yupo tayari kumpisha mgombea yeyote kutoka chama chochote cha upinzani ambae ataonekana ni bora anayeweza kumshinda mgombea atakaye gombea kupitia CCM iwapo chama chake kitamuagiza afanye hivyo.
Alisema yeye hayupo juu ya chama chake. Kwahiyo atatii na kutekeleza maagizo ya chama. Ikiwamo hilo lakuachiana maeneo ya kugombea.
Kwamujibu wa kaimu msimamizi wa uchaguzi wa halmashauri ya manispaa ya Lindi, Baptist Kihanza alisema tangu tarehe ya kuanza kwa zoezi la kuchukua fomu (12.8.2020) hadi leo (19.8.2020) saa 10.00 alasiri waliochukua fomu kutaka wateuliwe kugombea ubunge katika jimbo la Mchinga ni wawili. Wakati katika jimbo la Lindi mjini ni watatu.
