Kwa mara ya kwanza leo Jumatatu Iran imethibitisha hadharani kwamba iko kwenye mazungumzo na hasimu wake katika ukanda huo wa Mashariki ya kati Saudi Arabia.
Jamhuri hiyo ya Iran imesema itafanya kila iwezalo kuyapatia ufumbuzi masuala yaliyoko baina yao.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Saeed Khatibzadeh akizungumza katika mkutano na waandishi habari wa kila wiki unaooneshwa kwenye televisheni amesema,nchi zote mbili na kanda nzima kwa ujumla zina maslahi ya kuona mivutano inaondoka baina ya nchi hizo za kiislamu zilizoko katika eneo la ghuba ya uajemi.
Wiki iliyopita balozi Rayed Krimly ambaye ni kiongozi wa mipango ya sera katika wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo baina ya nchi yake na Iran yanalenga kupunguza mivutano ya kikanda.
Kadhalika alisema ni mapema mno kuzungumzia matokeo na serikali ya Saudi Arabia inataka kuona kuona uthibitisho wa kivitendo.
