Borrell, Lavrov waelezea matumaini kuhusu mkataba mpya juu ya nyuklia ya Iran


Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema kuna dalili zinazoashiria uwezekano wa kupatikana kwa makubaliano mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. 


Akizungumza katika mji wa Brest nchini Ufaransa, Borrell amesema matumaini hayo yanatokana na mazingira chanya katika mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna, baina ya Iran na wadau wengine wa mpango huo. Amesema kazi kubwa inafanyika, na yumkini katika muda wa wiki chache zijazo matokeo ya mwisho yatajulikana. 


Matarajio mema kutoka mazungumzo hayo ya vienna yameelezewa pia na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, ambaye akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, amesema anaridhishwa na mwelekeo yanaouchukua. 


Lavrov amesema upo utashi wa dhati kati ya Iran na Marekani ya kupata muafaka, unaotilia maanani wasiwasi wa kila upande. Mbali na Iran na Marekani, nchi nyingine wadau katika mazungumzo hayo ni Urusi, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na China.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi