Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kumpata mwenyekiti wa tatu wa chama hicho Jumamosi wiki hii katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.
Awali chama hicho kilichosajiliwa mwaka 2014, kilimchagua Anna Mghwira kuwa mwenyekiti wake hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Juni 2017, ambapo Yeremiah Maganja akikabidhiwa kukaimu nafasi hiyo.
Machi 2020, Maalim Seif Sharif Hamad alichaguliwa kuongoza tena chama hicho hadi mauti ilipomfika Februari mwaka jana huku Doroth Semu akikabidhiwa kukaimu hadi Jumamosi wiki hii atakapopatikana mrithi.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema wajumbe 560 wa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho watashiriki kumchagua miongoni mwa wawili waliogombea.
Kauli hiyo ameitoa leo Januari 24, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati akitangaza ratiba za mkutano huo utakaotanguliwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
“Huu utakuwa ni mkutano unaotoa mwelekeo mpya wa chama ifikapo 2025. Ni tukio kubwa katika chama linaloendana na ajenda ya uchaguzi huo pamoja na uzinduzi wa program ya ‘ACT kiganjani’ na mfumo mpya wa kufuatilia uwajibikaji wa Serikali.” Wagombea wa uenyekiti ni Juma Duni Haji na Hamad Masoud Hamad wote kutoka Zanzibar.
Kuhusu mfumo
Katika hatua nyingine chama hicho kimeandaa mfumo utakaofuatilia utekelezaji wa majukumu ya Serikali ndani na nje ya Bunge.
Shaibu amesema mfumo huo utakaosaidia kuchochea kasi ya uwajibika wa serikali ni matokeo ya udhaifu wa Bunge kutotekeleza jukumu hilo.
“Tumebaini Bunge halisimamii ipasavyo serikali matokeo yake haiwajibiki kwa wananchi, mfumo huu tutakaozindua katika mikutano hiyo,” Shaibu.
Soma hapa: Othman Masoud atangazwa kuwa mrithi wa Maalim Seif
Mfumo huo ni sehemu ya ajenda tatu, nyingine zikiwa ni kujaza nafasi ya Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wa chama hicho pamoja na uzinduzi wa programu ‘ACT Kiganjani’ inayotoa mwelekeo mpya wa uendeshaji wa chama hicho kidigitali.