Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Watu wenye silaha wamkata kichwa mwanasiasa mwingine Nigeria

 


Watu wenye silaha kusini mashariki mwa Nigeria wamemuua kwa kumkata kichwa mwanasiasa mwingine katika jimbo la Anambra.


Msemaji wa polisi, Ikenga Torchukwu ameiambia BBC kuwa mwili wa Nelson Achukwu- mbunge wa zamani katika jimbo la Anambra ulipatikana Jumanne baada ya kutekwa nyara kutoka nyumbani kwake mapema mwezi huu.


Haijabainika ni nani aliyetekeleza utekaji nyara na mauaji ya mwanasiasa huyo mlemavu.


Ripoti zinaonyesha kuwa ilikuwa ni mara ya pili yeye kutekwa nyara katika miezi kadhaa na pesa ililipwa ili kuachiliwa wakati wa kutekwa nyara kwake mara ya kwanza.


Achukwu alikuwa mwanasiasa wa hivi karibuni kulengwa katika eneo hilo.


Mamlaka mara nyingi zimewalaumu watu wanaotaka kujitenga wanaodai jimbo lililojitenga la Biafra kwa ghasia zinazozidi kuwa mbaya kusini mashariki mwa Nigeria.


Kukatwa vichwa na watu wenye silaha kunazidi kuwa kama mtindo wa sasa katika eneo hilo.


Hivi karibuni mbunge wa eneo hilo na msaidizi wake pamoja na afisa wa kijeshi na mwenza wake wa kike pia walikatwa kichwa.


Nigeria inakabiliana na ghasia zisizokwisha zinazofanywa na makundi mbalimbali yenye silaha kote nchini.


Hali ya ukosefu wa usalama inazidi kuwa mbaya wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika Februari mwaka ujao.

Post a Comment

0 Comments