Ticker

6/recent/ticker-posts

Mtoto wa Desmond Tutu azuiwa kuendesha ibada ya mazishi kutokana na ndoa yake ya jinsia moja

 

Mtoto wa marehemu Desmond Tutu amezuiwa na Kanisa la Uingereza kuongoza mazishi kwa sababu ameolewa na mwanamke.


Mpho Tutu van Furth ni kasisi wa Kianglikana katika Dayosisi ya Washington na alikuwa ameombwa kuongoza mazishi ya marehemu baba yake wa imani, Martin Kenyon, huko Shropshire siku ya Alhamisi.


Bi Tutu van Furth aliambia BBC kwamba "Hatua hiyo ni mbaya na imemuumiza’’.


Kanisa la Anglikana haliruhusu makasisi wake kuwa katika ndoa ya watu wa jinsia moja kwa sababu fundisho lake rasmi ni kwamba ndoa ni kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja.


Hata hivyo kanisa dada la Anglikana nchini Marekani, The Episcopal Church, wanaruhusu makasisi kuingia katika ndoa za jinsia moja.


"Ushauri ulitolewa kulingana na mwongozo wa sasa wa Baraza la Maaskofu kuhusu ndoa za jinsia moja," taarifa kutoka Dayosisi ya Hereford ilisema.


Askofu wa zamani wa Liverpool, Mchungaji Paul Bayes, ambaye ni mwanaharakati wa kanisa kubadili msimamo wake , alisema "tunahitaji mabadiliko".


"Tunahitaji kwa haraka kutengeneza nafasi kwa ajili ya dhamiri, nafasi kwa ajili ya uchungaji, na nafasi ya upendo," alisema.Baada ya familia ya Bw Kenyon kuambiwa uamuzi wa Kanisa, walihamisha ibada ya mazishi kutoka St Michael and All Angels huko Wentnor, karibu na Bishops Castle, hadi kwenye jumba la kasri la karibu ili Bi Tutu van Furth aweze kuongoza na kuhubiri.


"Inasikitisha sana," Bi Tutu aliambia BBC . "Inahisi kama jibu la ukiritimba na labda ukosefu wa huruma.


Baba yake Desmond Tutu, aliyefariki Desemba 2021, alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1984 kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Pia alifanya kampeni kuunga mkono haki za wapenzi wa jinsia moja na kuunga mkono ndoa zao.

Post a Comment

0 Comments