F Bilioni 41.1 kusambaza maji wilaya ya Mbulu | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Bilioni 41.1 kusambaza maji wilaya ya Mbulu


Na John Walter -Mbulu

Ile adhma ya Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kumtua ndoo mama kichwani kwa kumsogezea huduma ya maji safi na salama Karibu, inazidi kuzaa matunda ambapo Vijiji 21 katika halmashauri ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara vinatarajiwa kunufaika na mradi mkubwa wa maji wa Dambia -Haydom wa Bilioni 41.1 ifikapo Oktoba 15, 2025.

Mradi huo ambao upo chini ya mkandandarasi KINGS BUILDERS LIMITED  ya Dar es Salaam kwa usimamizi wa Wakala wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Manyara,  umefikia asilimia 10 ya utekelezaji.

Meneja RUWASA wilaya ya Mbulu Mhandisi Onesmo Mwakasege, amesema wamechimba Visima vitatu vyenye uwezo wa kutoa zaidi ya lita laki mbili kwa saa huku wakiendelea na ujenzi wa matenki mawili ya ujazo wa lita laki 5, nyumba ya mitambo na tenki kubwa lenye uwezo wa kubeba lita milioni mbili.

Mhandisi Mwakasege amesema watakuwa na mtandao wa mabomba yanayosambaza maji katika vijiji 20 wenye urefu wa kilomita 356, Ujenzi wa vituo 192 ambavyo vitafungiwa mfumo wa malipo kabla yaani (Pre paid water meter),  ujenzi wa ofisi ya chombo ambacho kitasimamia uendeshaji wa mradi, nyumba ya mlinzi na vinywesheo maji vinne kwa ajili ya mifugo.

Katibu wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Ndugu Iddi Mkowa akiwa na wajumbe  wengine wa Kamati ya siasa  kwenye ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, wamekagua mradi huo mkubwa wa maji wa Dambia-Haydom ambapo ameielekeza RUWASA kuhakikisha waliopitiwa na mradi wanalipwa fidia zao kabla ya juni 30, 2024 ili kusiwepo na vikwazo.



Akizungumza na Wananchi wa Dambia, Dirim na Yaeda kati, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mheshimiwa Queen Sendiga,  amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila Mwananchi mjini na vijijini anapata huduma ya maji safi na salama.

Aidha amemuomba Waziri wa Maji Mhe.Juma Aweso kukamilisha mpango wa upatikanaji  fedha kwa wakati kwa ajili ya kumlipa mkandarasi anaetekeleza mradi huo wa kimkakati.

Amesema katika mwaka wa fedha unaomalizika, kwenye miradi ya maji pekee mkoa mzima ukiacha miradi ya kimkakati, kwenye miradi midogo midogo wamepokea zaidi ya Bilioni 21 huku wakitarajia kupokea bilioni 19 kwa mwaka wa fedha ujao.



“Niwaombe Wananchi kutokufanya uharibifu kwenye maeneo ya vyanzo na kulinda na kutunza miundombinu hii idumu kwa muda mrefu.”amesema Sendiga.

Mradi huo utakapokamilika utawanufaisha Wananchi 133,737 sawa na ongezeko la asilimia 56.1 la upatikanaji wa huduma ya maji wilaya ya Mbulu.

Post a Comment

0 Comments