Na John Walter-Babati
Madereva wanaotumia barabara kuu ya Babati–Arusha wamepongeza ujenzi wa Daraja la Mto Mulungu lililopo eneo la Minjingu wilayani Babati mkoani Manyara, wakisema daraja hilo limeondoa kero kubwa iliyokuwepo kipindi cha mvua ambapo barabara hiyo ilikuwa haipitiki. Kwa sasa, madereva na watumiaji wengine wa barabara wanapita kwa uhuru na usalama zaidi.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanywa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, aliyekagua na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo ambalo limekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 6 kupitia mpango wa dharura wa serikali.
Daraja la Minjingu lina urefu wa mita 50 na kina cha mita 6, na ni mojawapo ya madaraja matano mapya yaliyojengwa mkoani Manyara kufuatia athari za mvua za El Niño zilizonyesha mwaka 2023. Kwa ujumla, madaraja hayo yamejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 19.8.
Mhandisi Kasekenya amempongeza mkandarasi mzawa, Rocktronic, kwa kutekeleza mradi huo kwa ubora unaokidhi viwango na kwa kukamilisha kazi kwa wakati. Aidha, ameielekeza TANROADS mkoa wa Manyara kuendelea kuimarisha kingo za daraja pamoja na kuweka taa za barabarani ili kuhakikisha usalama na uimara wa daraja hilo kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha ujenzi wa madaraja zaidi ya 80 katika mikoa 22 nchini kupitia mpango wa dharura, hatua iliyosaidia kuboresha miundombinu na kurahisisha usafiri hasa katika maeneo yaliyokumbwa na maafa ya mvua.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Manyara, Mhandisi Amon Mngulu, amesema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Minjingu, wanaendelea na kazi ya kufungua mto pande zote pamoja na kulinda kingo zote za daraja ili kulizuia kuathiriwa na mafuriko siku zijazo.


0 Maoni