Maboresho Bandari ya Tanga yaimarisha uchumi wa buluu

 


Na Rebeca Duwe, Tanga


MABORESHO ya miundombinu ya Bandari ya Tanga yaliyofanywa na Serikali yameelezwa kuwa ni miongoni mwa hatua muhimu katika kukuza usafiri wa majini na kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.


Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Musa Mandia, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Tanga.


Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Zanzibar (ZDMA), kwa lengo la kuonyesha mchango wa usafiri wa majini katika biashara, ajira na maendeleo ya nchi, pamoja na kusisitiza umuhimu wa usalama wa maisha katika shughuli za usafiri wa majini.


Mandia alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo imejikita katika wito wa kuimarisha utekelezaji wa sera na viwango vya ubora katika sekta ya bahari.


Alisema umuhimu wa maandalizi na uwepo wa vifaa vya utafutaji na uokoaji umeonekana kupitia mazoezi yaliyofanyika wakati wa maadhimisho hayo, ambayo yamelenga kuhakikisha wahusika wanakuwa tayari kuchukua hatua pindi ajali au hatari inapotokea baharini.


“Zoezi hili linaonyesha kwa vitendo thamani ya vifaa, kanuni na mipango ya utafutaji na uokoaji katika kuhakikisha watu wako tayari kuchukua hatua pale hatari inapotokea katika usafiri wa majini,” alisema.


Maonyesho ya utafutaji na uokoaji yalifanyika katika eneo la Raskazone Swimming Pool jijini Tanga na kushuhudiwa na wakazi wa jiji hilo.


Katika zoezi hilo, nahodha alitoa amri kwa watu kuondoka kwenye chombo kilichokuwa katika hatari ya kupata ajali, huku timu ya uokoaji ya TASAC 1 ikifika na kuwasaidia watu waliokuwa kwenye chombo hicho.


Mandia alisema Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda maisha ya watu baharini, ikiwamo Mkataba wa Kimataifa wa Utafutaji na Uokoaji Baharini wa mwaka 1979 (SAR Convention), pamoja na mikataba mingine ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO).


Alisema Serikali imeendelea kuonyesha umuhimu wa kuboresha miundombinu ya Bandari ya Tanga kutokana na ongezeko la usafirishaji wa abiria kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.


Kwa mujibu wa Mandia, Serikali tayari imenunua boti nne za utafutaji na uokoaji, ambazo zimepelekwa katika maeneo mbalimbali, yakiwamo Tanga, Kigoma na Dar es Salaam, huku pia zikiwa zipo boti nne za doria.


Awali, Mwenyekiti wa Maadhimisho hayo, Stella Katondo, alisema utafutaji na uokoaji ni sehemu muhimu ya usalama wa maisha ya binadamu katika usafiri wa majini.


Katondo alisema Tanzania imeingia katika mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kuhakikisha usalama wa binadamu unakuwa kipaumbele katika shughuli za usafiri wa majini.


Alisema zoezi la utafutaji na uokoaji lililopewa jina ‘Abandon the Ship’ lililenga kuonyesha hatua zinazopaswa kuchukuliwa wakati chombo kinapopatwa na maafa na abiria wanahitaji kuokolewa.


Alisema vifaa vinavyotumika katika uokoaji ni pamoja na jaketi za kuokoa maisha (life jackets), boti za kuokoa maisha (lifeboats) na maboya ya uokoaji (life rafts).


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi