Na Rebeca Duwe, Tanga
JITIHADA za kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya katika Jiji la Tanga zinaelekezwa zaidi katika utoaji wa elimu, ushirikishwaji wa jamii na uwezeshaji wa wadau, huku viongozi wakisisitiza kuwa mapambano dhidi ya tatizo hilo yanahitaji mshikamano wa jamii nzima.
Wito huo umetolewa na Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Khalid Rashid, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya yaliyowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wahudumu wa afya, maafisa maendeleo ya jamii, walimu na vijana.
Rashid amesema Jiji la Tanga limejipanga kuimarisha juhudi za kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuongeza utoaji wa elimu na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, hatua inayolenga kuwalinda vijana dhidi ya madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Amesema nafasi ya jamii katika mapambano hayo ni muhimu, akieleza kuwa jiografia ya Tanga, ikiwemo ukaribu wake na nchi jirani ya Kenya pamoja na eneo lake la mwambao wa Bahari ya Hindi, inahitaji ushirikiano wa karibu katika juhudi za kudhibiti uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
“Tatizo la dawa za kulevya hatutengenezi sisi, zinatoka nje. Tanga tumepakana na nchi jirani ya Kenya, ambayo ni sehemu inayotuathiri, na pia tupo mwambao wa bahari, ambao kwa mujibu wa tafiti unaweza kutumika kama njia ya kuingiza dawa hizo. Tunashirikiana sana na jamii kwa sababu waathirika wakubwa ni wanajamii, na jambo hili linatuumiza sana sisi kama viongozi,” amesema Rashid.
Amesisitiza kuwa juhudi za viongozi na taasisi zinazohusika haziwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila ushiriki wa wananchi, akiwataka kushirikiana na vyombo husika kwa kutoa taarifa na kuunga mkono hatua zinazolenga kuzuia usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya.
WADAU 22 KUPATIWA MAFUNZO
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Shirika la Gift of Hope, Said Bandawe, amesema washiriki 22 wanapatiwa mafunzo ya kinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya kwa muda wa siku tano, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii katika maeneo yao.
Bandawe amesema washiriki hao wanatarajiwa kutumia ujuzi watakaoupata kuwaelimisha wananchi wengine baada ya kukamilisha mafunzo hayo, hatua inayolenga kupanua wigo wa uelewa wa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na namna ya kuyazuia.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yanatekelezwa kupitia mradi wa “Focus on Youth, Not Substance” unaotafsiriwa kwa Kiswahili kama “Tuzingatie Vijana, Siyo Dawa za Kulevya.”
Amesema mradi huo unalenga kupunguza unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya vijana wanaotumia dawa za kulevya, kupunguza madhara yanayotokana na matumizi hayo na kuimarisha juhudi za kuwafikia na kuwasaidia vijana walio katika hatari ya kuanza au kuendelea kutumia dawa hizo.
Aidha, mradi huo unatumia ushirikishwaji wa jamii, utoaji wa elimu na kampeni za uhamasishaji kama njia za kuongeza uelewa na kuimarisha kinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, hususan miongoni mwa vijana.
Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa kushirikiana na programu ya Tanga Yetu, inayofadhiliwa na Foundation Botnar na kutekelezwa na Innovex kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Juhudi hizo zinalenga kuimarisha mazingira yanayowezesha vijana kulindwa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya, kupata fursa za maendeleo na kushiriki kikamilifu katika kujenga jamii yenye afya na ustawi.
