WATUHUMIWA WA MAUAJI WAKAMATWA MKOANI TANGA

 


 Na Rebeca Duwe Tanga 


Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za mauaji katika matukio mawili tofauti yaliyotokea Wilaya za Muheza na Handeni, mkoani Tanga.


Katika tukio la kwanza, Jeshi la Polisi linamshikilia Mbaraka Athumani Mkomwa, mwenye umri wa miaka 28, kwa tuhuma za mauaji ya Jennifer Elias Kipingu, aliyekuwa mpenzi wake. Tukio hilo lilitokea tarehe 23 Septemba 2026, ambapo mwili wa marehemu ulikutwa katika bonde la Mto Mission, Kata ya Mlingano, Wilaya ya Muheza. Mauaji hayo yanadaiwa kuchochewa na wivu wa mapenzi.


Katika tukio jingine, watuhumiwa wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la mauaji lililoripotiwa tarehe 21 Oktoba 2026, katika Wilaya ya Handeni ambapo wanatuhumiwa kumuua Athuman  Juma Said Watuhumiwa hao walikamatwa tarehe 22 Oktoba 2026, katika Kitongoji cha Kwedigasu, Kijiji cha Mkata Mashariki, Kata ya Mkata, kufuatia msako uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi wenye weledi wa eneo hilo.


Watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi huku taratibu za upelelezi zikiendelea kukamilishwa. Pindi zitakapokamilika, watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.


Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutatua tofauti zao kwa njia za amani na kuepuka vitendo vya ukatili vinavyoweza kusababisha vifo. Vilevile, wananchi wanahimizwa kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu na viashiria vyake ili kulinda amani na usalama katika jamii.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi