Aliyekuwa kocha msaidizi wa klabu ya Simba, Irambona Masoud Djuma amekiri kuachana na Simba baada ya pande zote mbili kuafikiana kuvunja mkataba kwa maslahi ya klabu, huku akiwaahidi mashabiki kuwa huu sio mwisho bali ipo siku watamuona tena.
Akiongea jioni ya leo Oktoba 8, 2018 kwenye makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Msimbazi Dar es salam, Masoud ameweka wazi kuwa anawapenda sana mashabiki wa Simba huku akiitakia kila la kheri klabu hiyo.
''Nashukuru kwa nafasi niliyopewa ya kuwa Simba, sikuwahi kufikiria nitaipata lakini imetokea, ila kila lenye mwanzo lina mwisho nafikiri tumeishia hapa kwasasa ila sio mwisho naamini ipo siku mtaniona tena mashabiki wa Simba nawapenda sana na nawatakia jema kwenye ligi na michuano ya kimataifa'', amesema Masoud.
Kwa upande wake Kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah, amesema wao kama klabu wanaheshimu ubora na mchango wa Masoud kwenye klabu yao hivyo wataendelea kumkumbuka na wao wanaamini hata yeye ataendelea kutoa nguvu kwa Simba kwasababu wamemalizana vyema.
