Maajabu! Mwanamke aweka rekodi nzito, ni baada ya kujioa mwenyewe


Mwanamke mmoja nchini Uganda ameshangaza wengi baada ya kujioa mwenyewe.

Lulu Jemimah mwenye umri wa miaka 32 alijioa mwezi Agosti jijini Kampala na kudai kuwa kwa miaka kadhaa watu wamekuwa wakimuuliza kuwa lini angefunga ndoa.

"Nikiwa na miaka 16 baba yangu aliandika hotuba yake kwa ajili ya kuisoma siku ya harusi yangu. Kila nilipokuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa mama yangu alikuwa akiniombea, na kwa miaka ya karibuni maombi yake yalikuwa pamoja na kupata mume bora, ambaye atanifaa," amesema Jemimah.

Mwaka jana Jemimah alichaguliwa kujiunga na masomo ya juu ya uandishi wa ubunifu katika chuo kikuu maarufu cha Oxford nchini Uingereza. Lakini licha ya mafanikio hayo ya kielimu anasema bado watu waliendelea kumuuliza anapanga kuolewa lini, ili aanzishe familia na kupata watoto.

"Hawaamini kuwa kinachonifanya kuwa macho usiku sio hofu ya uwezekano wa kutopata bahati ya kutembea altarini kwenda kufunga ndoa."

Kutokana na hali hiyo, Jemimah anasema aliamua kuchukua uamuzi wa kuwatuliza; "Nilipotimiza miaka 32 nikaamua kujioa. Naamini mimi nitajitunza na kujipa amani."

"Rafiki yangu mmoja aliniazima gauni la harusi, mwingine akijitolea kuniremba. Dada yangu aliniazima vito na kaka akaoka keki."


Waalikwa wote walielekezwa wapi pa kwenda na huko walitakiwa wajilipie gharama za vinywaji na chakula kwa pesa zao.

"Ndoa ni kielelezo cha upendo na msimamo thabiti wa maisha. Lakini kwa watu wengi nyumbani (Uganda) ni njia pekee ya mwanamke kujihakikishia usalama wa kifedha. Hata mie nahitaji hivyo vitu, lakini tofauti pekee hapa ni kuwa nitajipatia mimi mwenyewe."

Jemimah ameandika maelezo hayo ya maisha yake katika ukurasa wa mtandao wa kukusanya pesa kwa watu wenye uhitaji unaofahamika kama Go Fund Me.


Mpya zaidi Nzee zaidi