Safari Stars AFCON itakavyoanza kesho

KESHO timu ya Taifa, Taifa Stars inarudiana na wenzao wa Cape Verde kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na huenda ukawa mchezo wa kuamua kama itakwenda AFCON mwakani nchini Cameroon ama la.

Ni baada ya kuchapwa mabao 3-0 Jumamosi iliyopita nchini Cape  Verde, kipigo ambacho hakikutarajiwa na Watanzania wengi.

Ni mechi ndiyo inayoonekana kutoa taswira kama Stars itafuzu AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 38 au la.

Wakati Watanzania wanajipanga kesho kwenda kuishangilia Stars, lakini bado taswira ya kipigo cha mabao 3-0 hakijawatoka kichwani.

Mashabiki wengi wamekuwa wakilaumu safu ya ulinzi na kiungo kuwa kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyosababisha timu hiyo ishindwe kupata matokeo kwenye mechi hiyo.

Mchezaji na kocha wa zamani wa Taifa Stars, Abdallah Kibadeni amesema kuwa nafasi ya Stars kushinda ipo, lakini kama kuna baadhi ya vitu vitarekebishwa.

"Nadhani tungeweka viungo wabunifu na wazoefu kwenye mechi ya marudiano. Nilichokiona, tulikosa aina fulani ya viungo kama Jonas  Mkude na mtu mbunifu kati kama Shiza Kichuya ili kuifanya ngome ya  timu pinzani kutikisika, hatukuwa na watu wenye uwezo wa kuitikisa  ngome ili kuwapa nafasi washambuliaji wetu kuipata mipira wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga," alisema Kibadeni.

Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike akiiongoza Taifa Stars kwa mara ya pili tangu aanze kazi Agosti mwaka huu, alifanya mabadiliko ya  mapema tu dakika ya 38 akimtoa beki wa kushoto, Gardiel Michael na  kumuingiza beki wa kulia Shomari Kapombe.

Pamoja na Kapombe kufanya vema, baadhi ya mashabiki wakadai kuwa aliyekuwa anatakiwa kufanyiwa mabadiliko alikuwa ni Hassan  Kessy ambaye alishindwa kumkaba winga wa kushoto wa Cape Verde aliyekuwa akifanya anavyotaka.

Wengine wakadai kuwa kocha alikuwa amekariri kikosi kile ambacho kilitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Uganda ugenini, hivyo akakiamini bila ya kufanyia marekebisho kidogo.

"Kweli matokeo kwetu hayakuwa mazuri na kitu ambacho tumekosea ni kutowaheshimu wenzetu tuliokwenda kucheza nao," anasema Abdi Banda mchezaji wa Stars, anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika  Kusini kwenye timu ya Boroka FC.

"Unajua wenzetu wale hata kwa kiwango cha soka wako juu yetu,  lakini sisi inaonekana tulikwenda na matokeo kichwani kutokana na mechi ya Uganda. Lakini kwa sababu wao walijipanga na sisi  tutajipanga kwenye mechi ya nyumbani, tunaweza kufanya vizuri,"  alisema Banda.

"Sisi tuliingia na mipango yetu ilikuwa ni kuzuia zaidi na kushambulia kwa kushtukiza kwa sababu tuko ugenini, huwezi kujiachia sana na  kushambulia muda wote, lakini kuna makosa tuliyafanya wenzetu wakayatumia," anabainisha Simon Msuva, kiungo anayecheza soka la  kulipwa nchini Morocco kwenye klabu ya Diffa El Jajida.

Ramadhani Kessy kwa upande wake anasema kuwa ilionekana ni mechi ya kwaida, lakini kilichowapa wakati mgumu ni baada ya  wapinzani wao kupata matokeo ya haraka haraka.

"Mabao ya haraka  ndiyo yaliyofanya baadaye mechi ikawa ngumu  kwetu." alisema.

Mechi ya kesho itaanza saa 11:00 na ili safari ya Stars kwenda AFCON iwe bado ipo ni lazima ishinde mechi hiyo ili ifikishe pointi tano,  vinginevyo itakuwa kama imejiengua yenyewe kwani tayari Uganda  imeshafikisha pointi saba baada ya kuitwanga Lesotho mabao 3-0  mwishoni mwa wiki.
Mpya zaidi Nzee zaidi