Shirika la fedha la kimataifa IMF limesema vita vya kibiashara vilivyosababishwa na hatua ya Marekani kutangaza viwango vya ushuru pamoja na madeni makubwa vimeshusha uchumi wa dunia.
Ikitangaza utafiti wake wa hivi karibuni hii leo kuhusiana na hali ya uchumi duniani katika kuelekea mkutano wa kilele utakaofanyika Bali Indonesia, IMF imesema kukua kwa uchumi duniani kwa mwaka huu kutasalia katika kiwango cha asilimia 3.7 na kusalia katika kiwango hicho hapo mwakani.
Utafiti huo unaonesha kuwa kiwango hicho ni cha chini kulinganisha na asilimia 3.9 iliyotangazwa April.
Uchumi unaonekana kuporomoka na kuwa katika kiwango cha asilimia 3.7 alisema mchumi mkuu wa IMF Maury Obstfeld wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kutangazwa kwa ripoti hiyo.
Aidha IMF imesema kiwango cha kukua kwa uchumi wa mataifa ya China na Marekani yaliyo na uchumi mkubwa duniani nacho pia kimeshuka.
Uchumi wa China sasa unakadiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia 6.2 kwa mwaka 2019 kiwango ambacho ni cha chini kulinganisha na asilimia 6.4 iliyokadiriwa Julai huku IMF ikionya uchumi wa China uko hatarini kuporomoka kwa asilimia moja kamili mwakani kama vita hivi vya kibiashara vitaendelea hali inayoleta hofu na kupunguza imani kwa wafanyabiashara na hivyo kuathiri masoko.
Kwa mujibu wa IMF utafiti huo hauhusishi athari ya viwango vingine vya ushuru dhidi ya China vinavyotarajiwa kutangazwa na Marekani pamoja na hatua zitakazo chukuliwa na China kibiashara dhidi ya Marekani .
