Wataalamu wa mazingira Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na viongozi wa kata ya Ntyuka, wameendesha msako wa kuwabaini watu wanaochimba mchanga na kusafirisha usiku kwenye eneo la Chidachi lililozuiliwa kutokana na uharibifu wa mazingira.
Maofisa hao walifanya msako huo jana kwa kukagua risiti za malipo ya vifusi vya mchanga kwenye viwanda vya tofali vilivyopo kata hiyo ili kubaini watu hao.
Akizungumza katika msako huo, Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, alisema wamebaini kuna baadhi ya watu wanaomiliki viwanda wanakula njama na wamiliki wa malori kwa kusafirisha mchanga na kuumwaga mwenye viwanda vyao nyakati za usiku.
“Operesheni hizi zitafanyika mara kwa mara kwa lengo la kukagua risiti za ununuzi wa mchanga kutoka kwa wamiliki wa malori ya kubeba mchanga,”alisema.
Kimaro aliagiza wafanyabiashara wote wenye viwanda vya tofali na wananchi wanaofanya ujenzi wahakikishe wanachimba mchanga maeneo yaliyoruhusiwa ambayo ni Zuzu, Mtumba, Ihumwa, Iyumbu na Mpunguzi na watu wote wahakikishe wanapatiwa risiti halali kuepuka kuchukuliwa hatua.
Alisema jiji hilo linatekeleza agizo la Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alililowaagiza kutunza mazingira.
Naye, Diwani wa Kata ya Ntyuka, Theobart Maina, alisema zaidi ya hekta 20 zimeharibiwa vibaya na wachimbaji wa mchanga likiwamo eneo la ukanda wa kijani.
“Kwa kutambua umuhimu wa eneo hilo tutafanya doria za mara kwa mara zitaendelea kufanyika ili kuwadhibiti wezi wa madini, ujenzi hasa nyakati za usiku,”alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Vestina Manota, aliwataka wamiliki wa viwanda vya tofali kuhakikisha wanachukua taarifa za watu wanaowauzia mchanga kwa kuandika jina la dereva na namba ya simu, namba ya gari lililobeba mchanga na nakala ya risiti za malipo ya ushuru.
Kadhalika, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Chidachi, Merina Nzunda, alisema wataendelea kufanya doria katika eneo hilo kila siku na kupita katika viwanda vya tofali kukagua risiti na taarifa zote zitapelekwa kwa mtendaji wa kata.
