Sababu za majeruhi ajali lori la mafuta kuendelea kufariki


Idadi ya vifo vya ajali ya lori la mafuta iliyotokea Agosti 10  mkoani Morogoro, imefika 100  baada ya majeruhi watatu waliokuwa wakitibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kufariki dunia juzi, huku madaktari wakitoa sababu ya vifo hivyo kuendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma MNH, Aminiel Aligaesha, alisema waliofariki dunia ni Mazoya Sahani, Khasim Marijani na Ramadhani Mgwila.

Kwa upande wao madaktari bingwa wa upasuaji kutoka katika hospitali hiyo, walisema majeruhi hao wanaendelea kupoteza maisha kutokana na madhara makubwa waliyopata hasa katika mfumo wa hewa.

Akitoa ufafanuzi huo, mmoja wa madaktari hao, Dk. Laurian Rwanyuma, alisema majeruhi waliopelekwa hospitalini hapo walikuwa tayari wengi wao wamepata madhara kwa asilimia 80 hadi 90.

Dk. Rwanyuma alisema majeruhi hao walioungua kwa ndani wameathiriwa na moshi wa moto kwenye mfumo wa hewa na figo hali iliyosababisha kupumua kwa msaada wa mashine.

“Majeruhi walioletwa hapa walikuwa wameungua kwa sehemu kubwa kuanzia asilimia 80 hadi 90 na wengi walikuwa wameungua kwa ndani kutokana kuathiriwa na moshi wa moto.

“ Walioungua ndani wameathirika mfumo wa hewa na figo kutokana na hewa chafu ya carbon monoxide iliyoingia kwenye mapafu yao na ndiyo maana wengi wamekuwa wakiwekwa ICU ili kupata hewa safi ya oxygen,” alisema Dk. Rwanyuma.

Daktari mwingine bingwa wa upasuaji, Edwin Mrema, alisema majeruhi hao waliungua sehemu kubwa ya ngozi zao hali iliyosababisha kukosa kinga za mwili na pia mwili kupoteza maji mengi.

“Ngozi ndiyo kinga ya kwanza ya mwili ambayo inalinda mwili usipate madhara ya vijidudu, na tukumbuke tu kuwa wagonjwa walioungua ngozi ikiwa wazi kinga ya mwili inapotea, hivyo kusababisha mwili kushambuliwa kirahisi.

“Tunaendelea kufanya upasuaji kwa majeruhi wa ajali ya moto, shida kubwa ni kwamba walipoungua ngozi walikosa kinga kwani ngozi inakinga mwili na pia wanapoteza maji mengi, ndiyo maana wanahitaji kuongezewa damu nyingi na vifaa vya kuwaongezea joto,” alisema Dk. Mrema.
Mpya zaidi Nzee zaidi