Na Thabit Madai,Zanzibar
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Khatib Hassan amewataka wajumbe wa kamati ya uongozi, usimamizi na udhibiti wa ujenzi Zanzibar (DCU) kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi mazuri ya ardhi unaofuata mipango miji.
Hassan ameleza hayo wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kamati ya uongozi wa usimamizi na udhibiti ujenzi wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020 wenye lengo la kujuadili shughuli za kamati hiyo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za baraza la manispaa ya magharibi B Mombasa Unguja.
Amesema wananchi wanahitaji kupewa maelekezo juu ya matumizi mazuri ya ardhi ili kupunguza ujenzi usiozingatia mipango miji na kusisitiza kuwa serikali ya mkoa haitohusika katika uvunjaji wa majengo yaliyojengwa kinyume na utaratibu wakati mamlaka husika hazikusimamia na kutekeleza vyema wajibu wake.
“Sisi uongozi wa serikali ya mkoa hatutahusika katika kuwabomolea wananchi wetu wakati tangu wananza kujenga katika sehemu zisizokuwa rasmi sheha wa shehia husika,diwani na DCU wote walikuwepo hawakuchukua hatua angalau ya kuzua ujenzi”alisema Mhe Hassan.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewaomba wajumbe wa kamati hiyo kutoa ushauri kwa taasisi husika kurejeshwa serikali viwanja vyote ambavyo vimekaa kwa muda mrefu bila ya kuendelezwa ili vitumike kwa shughuli za maendeleo.
“Kumekuwa na viwanja vingi katika maeneo mbali mbali ya mikoa yetu vimekaa kwa muda bila ya kuendeleza lakini nyinyi kama wasimamizi na watoa vibali mmekaa kimya hatujashauri serikali vikarudishwa kwa ajili ya matumizi mengine”alisema mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo Hassan ameitaka kamati hiyo kushirikiana na taasisi nyengine za serikali katika kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha sera,sheria na taratibu za matumizi ya ardhi zinatumika vizuri.
Kikao hicho cha kamati ya uongozi ya usimamizi na udhibiti ujenzi Zanzibar DCU kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa kazi zake pia kilipata kuangalia rasimu ya muongozo wa utoaji vibali na udhibiti wa ujenzi.
