Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ametoa msaada wa gari kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Ndwika iliyopo wilayani Masasi kwa ajili ya kutatua tatizo la usafiri kwenye shule hiyo ambalo limedumu kwa muda mrefu.
Mapema kwa mwaka huu Mkuu wa Mkoa huyo alifanya ziara katika shule hiyo na kuelezwa uwepo wa changamoto hiyo gari la kusafiria ikiwemo kubeba wanafunzi pale wanapopatwa na homa na kuhitaji kwenda hospitalini.
Hafla ya kukabidhi gari hilo aina ya Nissan ilifanyika jana katika viwanja vya shule hiyo na kuudhuliwa na viongozi wa serikali na binafsi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo, Byakanwa alisema amefarijika kutoa msaada wa gari hilo kwa sababu ahadi yake inatimia ya kutatua changamoto ya gari la usafiri kwenye shule hiyo.
Alisema aliitoa ahadi hiyo baada ya kuguswa na uwepo wa changamoto hiyo ya ukosefu gari la usafiri ambapo ilipelekea wanafunzi ambao wanapatwa na homa inakuwa vigumu kupelekwa hospital kutokana na ukossefu wa gari.
Byakanwa alisema baada ya kuona changamoto hiyo katika shule kwa wananfunzi ofisi yake na jitihada zake mwenyewe aliamua kuhaangaika usiku na mchana ili kupata gari hilo na kulitoa shule hapo.
Alisema hivyo gari hilo litumike kama inavyokusudiwa na lisibadilishiwe matumizi likatumika tofauti na malengo mahususi ya matumizi ya shule.
Byakanwa alisema kazi ya kwanza ya matumizi ya gari hilo ni shughuli za shule ikiwemo wanafunzi kulitumia kwenda hospital pale wanapohitaji kufuata matibabu.
"Gari kwa sasa litasaidia kutekeleza shughuli zenu mbalimbali za shule ambazo zilikuwa zinakwama kama kusafiri kwenda mjini ila nawaomba muitunze ili iweze kuduma," alisema Byakanwa
Hata hivyo Byakanwa hakutaja thamani ya gari hilo na kueleza kuwa kikubwa ametimiza ahadi yake hiyo kusaidia gari HIYO.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Pauline Ndomba alisema uongozi wa shule na wanafunzi kwa ujumla.
wanamshukuru mkuu wa Mkoa huyo kwa kuwapatia gari hilo.
Alisema kwa muda mrefu sasa wamekuwa katika mazingira magumu ya kusafiri pamoja na wanafunzi kushindwa kwenda hospitalini kwa wakati kutokana na ukosefu wa gari.
"Kwa niaba ya wanafunzi na uongozi wa shule ya Ndwika tunasema tunamshukuru mkuu wetu wa Mkoa kwa kutupatia msaada wa gari hili tulikuwa na shida kubwa ya gari," alisema Ndomba
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Changwa Mkwanzu alisema gari hilo litasaidia kuondoa adha ya wanafunzi kutumia usafiri WA bodaboda hasa nyakati za usiku.
