F ECLAT kutumia zaidi ya shilingi milioni 286 kujenga shule ya msingi Merekwa. | Muungwana BLOG

ECLAT kutumia zaidi ya shilingi milioni 286 kujenga shule ya msingi Merekwa.


Na John Walter-Manyara

Ni habari njema kwa wananchi wa Kata ya Dirma, Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, baada ya Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la ECLAT Development Foundation, Bw. Peter Toima, kutangaza rasmi kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Merekwa.

Akizungumza wakati wa kutangaza hatua hiyo, Bw. Toima amesema kuwa ujenzi wa awamu ya pili unatarajiwa kuanza mapema mwezi Februari, huku shule hiyo ikipangwa kukabidhiwa rasmi kwa Serikali tarehe 24 Novemba, 2026 baada ya kukamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, ECLAT Development Foundation inatarajia kutumia jumla ya shilingi 286,302,200 katika ujenzi wa awamu ya kwanza na ya pili ya shule hiyo, fedha zitakazogharamia ujenzi wa miundombinu muhimu ya elimu.

Shule ya Msingi Merekwa ikikamilika itakuwa na ofisi za walimu, madarasa yenye madawati, samani mbalimbali, jiko pamoja na matundu ya vyoo kwa walimu na wanafunzi, hatua itakayoboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Bw. Toima amesema kuwa falsafa ya shirika hilo ni “hawavumi lakini wapo”, akisisitiza kuwa ECLAT haifanyi kazi kwa ajili ya kujitangaza bali kwa dhati ya kuwahudumia wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.



Ameongeza kuwa hadi sasa, ECLAT Development Foundation imefanya kazi katika mikoa sita nchini, katika zaidi ya wilaya tisa, ambapo tayari zimeshajengwa takribani shule 60 za msingi, sambamba na ujenzi wa shule za sekondari katika maeneo mbalimbali.

“Kikubwa tunachoomba ni ushirikiano, umoja na kila mmoja kutimiza wajibu wake, ili maendeleo tunayoyataka yafikie jamii kwa haraka na ufanisi,” amesema Bw. Toima.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hanang’, Mheshimiwa Asia Halamga, amemshukuru kwa dhati Mkurugenzi wa ECLAT Development Foundation kwa uamuzi wa kujenga shule hiyo mpya ya msingi Merekwa, akieleza kuwa ni mradi wenye tija kubwa kwa jamii za pembezoni, hususan kwa watoto wa jamii za wafugaji ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya upatikanaji wa elimu.

Mheshimiwa Halamga amesema kuwa mchango wa ECLAT ni wa kupongezwa kwa kiwango kikubwa na unaonesha jinsi mashirika ya maendeleo yanavyoweza kushirikiana na serikali katika kufanikisha malengo ya elimu kwa wote.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bw. George Bajuta, ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya Halmashauri na Shirika la ECLAT Development Foundation, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokusudiwa.

Ujenzi wa Shule ya Msingi Merekwa unaendelea kuwa ishara ya matumaini mapya, ukithibitisha kuwa pale panapokuwepo na dhamira ya kweli, elimu inaweza kuwafikia hata watoto walioko maeneo ya mbali zaidi.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni