Na John Walter-Simanjiro
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Ndugu
Gracian Makota, amekutana na kufanya kikao kazi na wadau mbalimbali
wa uwindaji wa kitalii katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo, kwa lengo
la kujadili na kutafuta suluhu ya changamoto ya uvamizi wa vitalu vya uwindaji.
Kikao kazi hicho kilifanyika tarehe 27 Januari 2026
katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, na kiliwakutanisha wadau wa
sekta ya utalii wakiwemo Maafisa Kilimo, Maliasili na Mapato kutoka
ofisi ya Mkurugenzi, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini – Arusha, Mkuu
wa Utalii Kanda ya Kaskazini – Arusha, Maafisa Uhifadhi Wanyamapori,
pamoja na wamiliki wa vitalu vya uwindaji vya Ilaroi Ranching LTD,
Multicable Company LTD, Tanzania Big Game Safaris, Trophy Belt na Plains
Game Adventures.
Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kujadili namna bora ya kukabiliana
na changamoto ya uvamizi wa vitalu vya uwindaji, hali ambayo imekuwa
ikiathiri shughuli za uhifadhi na uwekezaji wa kitalii katika eneo hilo.
Baadhi ya wamiliki wa vitalu vya uwindaji wamesema
changamoto kubwa inayowakabili ni uvamizi unaofanywa na wananchi,
hususan wakulima, wanapoanza msimu wa kilimo.
Wamedai kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiingia hadi
ndani ya maeneo ya vitalu na kuanzisha mashamba mapya, hali inayosababisha wanyama
kukimbia maeneo hayo kutokana na hofu, jambo linaloathiri shughuli za
uwindaji wa kitalii na uhifadhi wa wanyamapori.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji Ndg.
Gracian Makota amesema kuwa miongoni mwa suluhu ya kudumu ya tatizo hilo ni
kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi maeneo jirani na vitalu
vya uwindaji.
Amesisitiza umuhimu wa kuitisha mikutano na vikao vya
kimkakati vitakavyowakutanisha wananchi hao ili kuwapatia elimu kuhusu faida
na umuhimu wa uwekezaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, ikiwemo ajira,
mapato ya Halmashauri na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imeeleza kuwa itaendelea
kushirikiana na wadau wa uhifadhi na utalii kuhakikisha changamoto hizo
zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa maslahi ya uhifadhi wa rasilimali za asili na
maendeleo ya wananchi.
@manyara_rs
@wizarayamaliasilinautalii
@ortamisemi
@tawa_tanzania
@gmakota

0 Maoni