F Polisi Wanawake mkoa wa Manyara wafanya utalii Tarangire. | Muungwana BLOG

Polisi Wanawake mkoa wa Manyara wafanya utalii Tarangire.


Na John Walter-Babati

Polisi wanawake mkoani Manyara wamefanya ziara ya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza utalii wa ndani na kuihamasisha jamii kutembelea vivutio vya asili vilivyopo nchini.

Ziara hiyo imeongozwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Christina Mkonongo kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF–Net) mkoani Manyara, akiwa ameambatana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati (OCD), Mrakibu wa Polisi (SP) Ernesta Mwambinga.

Katika ziara hiyo, viongozi hao waliwaongoza wakaguzi na askari wa kike kutoka Wilaya ya Babati pamoja na vikosi mbalimbali vya Polisi Mkoa wa Manyara, kwa lengo la kuonesha mfano kwa jamii juu ya umuhimu wa kushiriki utalii wa ndani, ambao una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, viongozi wa Polisi Wanawake wamesisitiza kuwa utalii wa ndani ni fursa muhimu kwa Watanzania kujifunza, kufurahia rasilimali zao za asili na kuchangia mapato ya taifa, huku wakihamasisha wananchi wa Mkoa wa Manyara na maeneo ya jirani kutembelea vivutio vilivyopo karibu nao.

Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, iliyopo Kaskazini mwa Tanzania mkoani Manyara, kando ya barabara ya Arusha – Babati, ni maarufu kwa makundi makubwa ya tembo, miti mikubwa ya mibuyu (baobab) pamoja na Mto Tarangire, ambao huvutia wanyama wengi hususan wakati wa msimu wa kiangazi.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano, ustawi wa askari wanawake pamoja na kuendeleza utamaduni wa kuthamini na kutangaza vivutio vya utalii wa ndani.


Chapisha Maoni

0 Maoni