Na John Walter-Manyara
Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, amekabidhi vifaa vya kufundishia kwa walimu wa elimu jumuishi katika Shule ya Msingi Magugu, wilayani Babati, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata nyenzo muhimu za kujifunzia.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Sillo amesema vifaa hivyo ni ishara ya dhamira ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuzingatia utu na kuhakikisha usawa wa elimu kwa makundi yote ya jamii.
Amewataka wanafunzi wa shule hiyo kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao.
Kwa mujibu wa Afisa Elimu Maalum wa Wilaya ya Babati, Glory Shilly, vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kompyuta mpakato (laptop) itakayowekewa programu ya sauti kwa ajili ya walimu na wanafunzi wenye uoni hafifu pamoja na vinasa sauti viwili (voice recorders) vitakavyosaidia katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.
Shule ya Msingi Magugu ina jumla ya wanafunzi 22 wenye mahitaji maalum wanaonufaika na mpango wa elimu jumuishi.
Diwani wa Kata ya Magugu, Stanley Charles, ameishukuru serikali kwa kuendelea kulijali kundi hilo muhimu, akisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum katika eneo hilo.
Shule ya Msingi Magugu ni miongoni mwa shule kongwe wilayani Babati, iliyoanzishwa mwaka 1954, na imeendelea kuwa kitovu muhimu cha utoaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wa kata hiyo na maeneo jirani.
