Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Harriet Rushekya, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza utalii endelevu nchini, akieleza kuwa mashindano makubwa ya kimataifa ya michezo kama Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanaweza kuwa fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali nchini.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka na Maonesho ya TASOTA Server Connect 2026, Rushekya ameipongeza Jumuiya ya Mawakala wa Usafiri Tanzania (TASOTA) kwa kuandaa jukwaa hilo muhimu linalowawezesha wadau wa sekta ya usafiri na utalii kujadili maendeleo, changamoto na fursa za kukuza biashara zao.
Amesema maendeleo ya teknolojia, yakiwemo matumizi ya akili unde (AI) na mifumo ya kidijitali ya kuhifadhi huduma za utalii, yanafungua milango mipya ya kibiashara kwa mawakala wa usafiri, lakini pia yanawaletea changamoto zinazohitaji ushirikiano ili kuhakikisha wadau wote wanakabiliana na mabadiliko hayo na kunufaika nayo.
Rushekya amebainisha kuwa Tanzania Destination Booking Platform, inayojulikana kama Travel Companion, ni miongoni mwa jitihada zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za utalii, kuboresha uzoefu wa wageni na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa. Amehimiza wadau kutumia teknolojia kuboresha huduma na kuendana na mahitaji ya soko la kisasa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia majukwaa makubwa ya michezo kama AFCON kutangaza vivutio vya Tanzania, kuimarisha utalii wa ndani na kuvutia wageni wengi zaidi. Ameeleza kuwa mafanikio ya utalii yanahitaji pia kulinda mazingira, kuhifadhi urithi wa utamaduni na kujenga ushirikiano imara kati ya Serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TASOTA, Talib Talib, amesema jumuiya hiyo inaendelea kuandaa mikutano na maonesho kwa lengo la kuwaunganisha mawakala wa usafiri na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri na utalii nchini. Amesema mikutano hiyo inatoa nafasi kwa wanachama kubadilishana taarifa, uzoefu na mawazo yanayoweza kusaidia kukuza biashara zao.
Talib amesema maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo HM, Galadina, Selcom na Shirika la Ndege la Air Tanzania, na kutoa fursa kwa mawakala wa usafiri kukutana na watoa huduma, kujenga mahusiano ya kibiashara na kutambua maeneo yanayoweza kushirikiana. Ameongeza kuwa mahusiano hayo ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kupanua wigo wa huduma zinazotolewa kwa wateja.
Kuhusu AFCON, Talib amesema TASOTA inaendelea kutathmini fursa zinazoweza kujitokeza kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafiri na utalii wakati wa mashindano hayo. Amesema jumuiya hiyo inalenga kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuweka mikakati itakayowawezesha mawakala wa usafiri kunufaika na fursa hizo, huku akisisitiza umuhimu wa ushiriki wenye usawa wa kijinsia.
Ameongeza kuwa TASOTA ina nafasi muhimu katika kupata na kusambaza taarifa za kibiashara kwa wanachama wake kupitia mahusiano yake na wizara na taasisi mbalimbali, ikiwemo TTB. Kwa mujibu wake, taarifa kuhusu mwenendo wa soko na wageni wanaoingia na kutoka nchini zinaweza kuwasaidia mawakala kufanya maamuzi sahihi, kuboresha huduma na kutambua fursa mpya za biashara.
Naye Omari Hamisi Kazimoto, Meneja na mchambuzi wa mifumo ya tiketi za ndege nchini Tanzania, amesema wadau wa sekta ya usafiri wa anga na utalii wameanza kujiandaa kupokea wageni wanaotarajiwa kuhudhuria AFCON. Amesema mashindano hayo yanaweza kuongeza mahitaji ya tiketi za ndege, malazi, usafirishaji na huduma nyingine, hivyo kutoa fursa kwa mawakala wa usafiri, kampuni za ndege, hoteli na wafanyabiashara wengine kupanua shughuli zao.
Kazimoto ameongeza kuwa ongezeko la wageni linaweza kuchochea mahitaji ya safari za ndege kati ya miji mbalimbali itakayohusishwa na shughuli za mashindano hayo, na hivyo kuongeza mzunguko wa biashara katika sekta ya usafiri na utalii. Amesema fursa hizo zinaweza pia kunufaisha sekta nyingine zinazotoa huduma kwa wageni, iwapo maandalizi yatafanyika kwa wakati na huduma zitaboreshwa kukidhi mahitaji ya soko.
Kwa pamoja, wadau hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha maandalizi na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha wageni wanapata huduma bora na fursa za kiuchumi zinazoweza kutokana na AFCON zinawanufaisha wadau wengi zaidi. TASOTA imesema itaendelea kuandaa mikutano na maonesho ya kila mwezi kwa lengo la kuimarisha mtandao wa wadau, kuongeza upatikanaji wa taarifa za kibiashara na kuwawezesha mawakala wa usafiri kutumia fursa za sekta ya usafiri na utalii kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.