Na. Thabit Madai Zanzibar
Hali ya upatikanaji wa Mafuta visiwani Zanzibar imekuwa tabu kwa baadhi ya vituo vya utoaji huduma hiyo kutokana na Kampuni ya United Petrolium (UP) kushindwa kuingiza mafuta kwa wakati ndani ya visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar ZURA kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mmlaka hiyol, Haji Kali Haji alisema tatizo hilo lipo na limesababishwa na ucheleweshaji wa kuingia kwa mafuta Zanzibar uliofanywa na kampuni ya Petrolium (UP)
Alisema ucheleweshaji huo unatokana na kampuni hiyo kupeleka meli ya United Spirit 1 ya nchini Msumbiji na kushindwa kuleta meli hiyo ya mafuta Zanzibar kwa wakati hali ambayo imepelekea kupungua kwa mafuta ya Petroli katika baadhi ya vituo vya mafuta hasa vituo vya Kampuni ya United Petrolium (UP).
Hata hivyo alieleza kwamba Kampuni ya Zanzibar Petrolium (ZP) na Kampuni ya GAPCO wameingiza mafuta nchini ambapo yanaendelea kusambazwa katika vituo vyao vya mjini na vijijini kuanzia asubuhi ya leo .
Alisema hali halisi ya uwepo wa mafuta nchini kwa kila kampuni ni kama ifuatavyo katika bohari kuu ya Mtoni leo Jumanne tarehe 5-3-209.
Kampuni ya GAPCO
- Petrol : Lita 942,317
- Diesal : Lita 799,629
- Kerosene : Lita 213,305
Kampuni ya ZANZIBAR PETROLEUM (ZP)
- Petrol : Lita 407, 415
- Diesel : Lita 904,688
- Kerosene : Lita 215,912
Kampuni ya UNITED PETROLEUM (UP)
- Petrol : Lita 98,152
- Diesel : Lita 205,505
- Kerosene: Lita 472,194
Aliendelea kusema jumla ya mafuta yaliopo nchini kwa sasa ni kama ifuatavyo.
Petrol Lita 1,447,884 sawa na matumizi ya siku tisa (9)
Dizeli Lita 1,909,822 sawa na matumizi ya siku kumi na mbili (12)
Mafuta ya Taa Lita 1,042,828 sawa na matumizi ya siku thalathini (30)
Pia alisema Kampuni ya United Petroleum (UP) inatarajia kuingiza mafuta kiasi cha tani 2.000 za Dizeli sawa na Lita 2,400,000 na Tani 1500 za Petroli sawa na Lita 2,047,500 kwa kutumia meli mpya ya mafuta ya East Wind II siku ya Ijumaa ya tarehe 8-3-2019 ambayo yatamaliza kabisa tatizo la uhaba wa mafuta nchini .
Aidha aliendelea kusema Kampuni ya Zanzibar Petroleum (ZP) inatarajia kuingiza mafuta kiasi cha Lita 1,600,000 za Petroli kwa kutumia meli ya East Wind I siku ya Jumapili ya tarehe 10-03-2019.
Hivyo alisema ZURA imesikitishwa sana na hali ya uhaba mdogo wa mafuta uliojitokeza hali ambayo imewasababishia wananchi kukosa huduma kwa kawaida.
Vile vile alieleza kwamba kutokana na hali hiyo ZURA imeyaagiza Makampuni ya Mafuta kuhakikisha kwamba yanasambaza mafuta kwa haraka na kurejesha huduma hiyo kwa wananchi na kuhakikisha inapatikana bila usumbufu.
Kwa hiyo ZURA inawaomba radhi wananchi wake kwa usumbufu uliojitokeza na kueleza kwamba inafuatilia kwa karibu matengenezo ya meli mbili zilizoharibika ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini inarejea kama kawaida.
Akitoa wito Mkurugenzi Haji alisema Mamlaka inawasisitiza wananchi kuacha tabia ya kusikiliza taarifa zisizo rasmi ambazo zinapelekea wananchi kuwa na taharuki katika upatikanaji wa huduma hiyo.
