Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi ya Wilaya ya Njombe imesogeza mbele kesi namba tatu ya mwaka 2019 inayowakabili washitakiwa watatu Mariana Malekela, Edwin Malekela na Kalistus Ndiungwa wanaokabiliwa na kosa la mauaji ya Mtoto Rachael Malekela mwenye umri wa miaka saba ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Matembwe, Tarafa ya Lupembe mkoani Njombe kwa imani ya kishirikina.
Washitakiwa hao watatu wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Njombe, Mheshimiwa James Mhanusi kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya pili, ambapo Hakimu Mhanusi ameahirisha shauri hilo hadi Machi 18, mwaka huu na kuamuru washtakiwa wote watatu warudishwe mahabusu.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Elizabeth Mally anayesimamia kesi hiyo kwa niaba ya Jamhuri ameiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo kwa sababu bado upelelezi haujakamilika.
Washitakiwa hao watatu wanadaiwa kuhusika na tukio la mauaji ya mtoto Rachel Malekela aliyekutwa ameuawa Februari Mosi, Mwaka huu katika Kitongoji cha Lung’angale, Kata ya Matembwe, Tarafa ya Lupembe, wilaya ya Njombe jirani na makazi ya nyumba yao.
Kuendelea kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao wa mauaji, ni jitihada za Jeshi la Polisi Mkoani Njombe zinazoendelea kuchukuliwa ili kuwabaini wahusika wa mauaji ya watoto wadogo yaliyotokea kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
