DC Masasi apiga marufuku kufanya kampeni za kisiasa kabla ya wakati



Na Hamisi  Abdulrahmani, Masasi

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, Selamani Mzee amepiga marufuku kwa kiongozi yeyote wa siasa wilayani humo kufanya kampeni za kisiasa kabla ya wakati kufika kwa ajili ya kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2020 badala yake wasubiri muda ufike ndipo wafanye hivyo.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amewapa rungu viongozi wa Serikali za mitaa wilayani humo kutofumbia macho vitendo vya baadhi ya wanasiasa wilayani  ambao watajitokeza na kupinga agizo hilo na kwamba vyombo husika vya sheria vitafanya kazi yake.

Mzee alitoa agizo hilo jana wilayani Masasi  wakati alipokuwa akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa serikali ya mtaa wapiwapi-A mara baada ya mkuu huyo wa wilaya kujitokeza katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Alisema katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 wa raisi, wabunge na madiwani wapo baadhi ya wanasiasa wilayani Masasi wameanza kufanya kampeni kwenye maeneo yao wakati wakifahamu muda wa kufanya hivyo bado haujafika.

Alisema wenyeviti, watendaji na wajumbe wa serikali za mitaa wilayani Masasi katika kutekeleza majukumu yao wasisite kutimiza wajibu wao kwa kudhibiti vitendo vya aina hiyo kwa baadhi ya wanasiasa ambao wameanza kujitokea kwenye maeneo mitaa yao na kufanya kampen za kisiasa za uchaguzi kabla ya wakati kufika.

Mzee alisema viongozi wa serikali za mitaa kwenye maeneo yao washirikiane kwa nguvu moja kuhakikisha wanasiasa hao wanawadhibiti kisha wanawachisha tabia hiyo na badala yake wanatakiwa kusubiri muda ufike ndipo wafanye kampeni hizo kupitia taratibu husika ikiwemo za vyama vyao.

Alisema kitendo cha kufanya kampeni kabla ya muda muhafaka kufika ni kujiondolea sifa stahiki ya kugombea pindi muda wa kufanya hivyo utakapokuwa tayari umefika.

Mzee alisema kufanya hivyo ni kuvunja taratibu husika za uchaguzi na kwamba vyombo husika vitawachukulia hatua stahiki za kisheria.

Aidha, Mkuu wa wilaya huyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa wilaya ya Masasi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kurekebisha taarifa zao kama zinauhitaji wa kufanya hivyo.

Kwa upande wake Msimamizi wa kituo hicho cha Mtaa wa Wapiwapi-A , Kulwa Mchelezo alisema zoezi hilo limeanza jana Januari 12 na hamasa ya watu kujitokeza kujiandikisha ni kubwa.

Alisema tangu zoezi hilo limeanza jumla ya watu 65 wamejitokeza huku zaidi ya wananchi 30 wakiwa ni wapya ambao umri wao kwa sasa unaruhusu kupiga kura.


Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ni kwa ajili ya wale wanaotaka kurekebisha taarifa zao kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupotelewa kadi zao, kuharibika na wale ambao kwa sasa wamefikisha umri wa kupiga kura na wanahitaji vitambulisho hivyo ili kuweza kupiga kura.