LAAC yashauri Halmashauri ya Dodoma kuongeza majengo Kituo Cha Afya Makole



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeishauri Halmashauri ya Jiji la Dodoma  kuyachukua majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Halmashauri ya Chamwino ili yawe sehemu ya  kituo Cha Afya Cha Makole ili kuondokana na ufinyu wa sehemu ya kituo hicho Cha Afya.

Ushauri huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota, (Mb) wakati Kamati hiyo ilipotembelea katika kituo hicho ikiwa ni sehemu ya ziara ya kukagua miradi iliyochini ya Kamati hiyo inayotekelezwa Jijini Dodoma, ambapo pia walitembelea Ujenzi wa Stendi kuu ya Mabasi Nanenane pamoja na Soko kuu.

Amesema moja ya  changamoto iliyopo kwa hospitali hiyo ni ufinyu wa eneo hivyo ni vyema wakaangalia namna ya kuchukua majengo hayo na kuyafanya kuwa ni sehemu ya kituo cha afya cha Makole.

“ Hapa inaonekana mnaufinyu wa eneo, na kwa sababu viongozi wote mpo, kwanini msiangalie uwezekano kuyachukuwa majengo yaliyokuwa yakitumiwa na Chamiwno na hiyo Shule ya Sekondari ya Viwandani ikaamishwa ili majengo na eneo hilo litumike na hospitali,”

Ambapo Katibu Tawala wa Mikoa wa Dodoma (RAS), Maduka Kessy, amesema wamepokea ushauri huo na kusema Kama uongozi wa Mkoa watakwenda kuliangalia suala hilo.

"Tumelipokea Kama uongozi wa Mkoa na sisi tutakwenda kukaa na kuliangalia swala hilo na kuja na maamuzi" amesema Maduka Kessy.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Makole, Dk George Matiko, amesema tangu kufanyia kwa uboreshaji wa kituo hicho uliofanyika baada ya Serikali kutoa Sh milioni 572, kumeboresha utoaji wa huduma za afya ikiwamo huduma ya mama na mtoto.

“ Huduma katika kituo chetu zimeimarika, kwa sasa oparesheni kwa mama wajawazito zimekuwa zikifanyika kwa mafanikio na tumepunguza vifo vya mama na matoto baada ya kujenga jengo ambalo lina vigenzo vinavyotakiwa kimataifa.” amesema Matiko.

Katika mradi wa Soko na Stendi ya mabasi, Mhandisi Mshauri Emmanuel Malimbo amesema ujenzi wa soko umefikia asilimia 87 na kuwa mkandarasi ameshalipwa asilimia 64 ya gharama za ujenzi huku ujenzi wa stendi ukifikia asilimia 85.

Naye Harish Jethwa kutoka Kampuni ya ukandarasi ya Mohammed Bulders, aliwahakikisha wabunge kuwa kazi hiyo itakamilika katika muda uliopangwa wa Februari 15.
Mpya zaidi Nzee zaidi