Marekani yatoa onyo kwa Iran kuhusu mkataba wa NPT

Mjumbe wa Marekani amesema leo kwamba kitisho cha Iran kujiondowa kwenye makubaliano ya kimataifa ya Nyuklia ikiwa nchi za Ulaya zitaifikisha Iran kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuitaja kwamba imekiuka makubaliano hayo ya mwaka 2015,kitatuma ujumbe mbaya kabisa.

Jana Jumatatu waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif alitowa ujumbe uliotangazwa na shirika la habari la Iran IRNA na mashirika mengine,akisema kwamba ikiwa Ulaya itaendelea na tabia yake isiyokubalika au kulipeleka faili la Iran mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,basi Iran itajiondowa kwenye mkataba huo wa NPT.

Mjumbe wa Marekani Robert Wood anayehusika na uondoaji silaha amesema mazungumzo yamepangwa kufanyika mwezi Aprili kuhusu mkataba wa NPT.

Mjumbe huyo akizungumza mjini Geneva mbele ya waandishi habari amesema Iran inapaswa kukomesha tabia yake ya vitisho na kukaa chini na Marekani kujadili makubaliano yatakayohusiana sio tu na suala la Nyuklia lakini na mambo mengine.
Mpya zaidi Nzee zaidi