Iran, Urusi, Uturuki zafanya mazungumzo ya amani ya Syria

Iran, Urusi na Uturuki, ambazo zinaunga mkono pande zinazozana katika vita vya Syria, zimefanya mazungumzo leo ya kuweka pamoja juhudi za kuleta amani katika nchi hiyo, ambayo mgogoro wake umeingia mwaka wa 10.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani amesema hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo wa Syria, wakati alipozungumza kwa njia ya video na wenzake wa Urusi na Uturuki.

Rais wa Urusi, Vladmir Putin ameshutumu vikwazo vilivyotangazwa upya na Marekani akisema vinalenga kuidhoofisha Syria, huku Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, akitoa wito wa amani na usalama kurejeshwa katika nchi hiyo ambayo ni jirani wake wa upande wa kaskazini.

Mazungumzo hayo ni ya kwanza tangu Septemba, katika kile kinachofahamika kama muundo wa Astana, ambao ni mazungumzo ya pande tatu ya mchakato wa amani kati ya madola muhimu ya kigeni yenye nguvu katika mgogoro wa Syria.