Polisi watumia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji huku kukiwa na taarifa kuwa baadhi yao wamejeruhiwa
Polisi nchini Myanmar katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw wametumia maji ya kuwasha dhidi ya wafanyakazi wanaofanya maandamano kote nchini humo dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.
Maelfu ya raia wanashiriki maandamano kwa siku ya tatu wakitoa wito wa kuachiwa huru kwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo Aung San Suu Kyi na kurejeshwa kwa demokrasia.
Hatua hiyo inawadia baada ya Myanmar kushuhudia maandamano makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi.
Wiki iliyopita, jeshi lilipindua serikali ya nchi hiyo baada ya kudai kwamba uchaguzi uliokuwa umefanyika awali, ulikumbwa na udanganyifu bila kutoa ushahidi wowote.
Pia jeshi lilitangaza hali ya tahadhari kwa kipindi cha mwaka mmoja nchini Myanmar ambayo pia inafahamika kama Burma, na mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing amechukua uongozi wa nchi hiyo.
Bi. Suu Kyi na viongozi waandamizi wa chama cha National League for Democracy (NLD), akiwemo Rais Win Myint, wamewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.
Kufikia Jumatatu asubuhi, makumi ya maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika katika mji wa Nay Pyi kushiriki maandamano huku miji mingine, Mandalay na Yangon pia nayo ikishuhudia maandamano hayo kulingana na idhaa ya BBC Burmese.
Waandamanaji ni pamoja na walimu, mawakili, maafisa wa benki na wafanyakazi wa serikali,
Takribani walimu elfu moja wamekuwa wakiandamana katika mji wa Yangon kuelekea Sule Pagoda kitovu cha mji mkuu wa Myanmar.
Hakuna taarifa zozote za ghasia zilizotolewa muda huo.
"Leo ni siku ya kufanyakazi, lakini hatutaenda kazini hata kama tutakatwa mshahara wetu," mwandamanaji mmoja, 28, anayefanyakazi katika kiwanda cha kutengeneza nguo, Hnin Thazin, amezungumza na shirika la habari la AFP.

0 Maoni