SAKATA la ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi Arusha limeibukia bungeni baada ya Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo, kuhoji Serikali ina mpango gani juu ya kujenga stendi ya kisasa jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi.
Stendi hiyo ambayo mchakato wake ulianza mwaka 2011 imekuwa na mvutano mkubwa na mwaka 2019 Gambo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisitisha mchakato wa stendi hiyo hadi pale masuala yanayoleta sintofahamu yatakapofanyiwa kazi.
Mwaka 2019 watendaji wawili wa Idara ya Mipango Miji na Uchumi, walisimamishwa kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk Maulid Madeni, kwa kile kilichoelezwa ni kupisha uchunguzi ujenzi Stendi ya mabasi eneo la Oloresho, Kata ya Olasiti.
Dk Madeni alisema ilibainika kuwepo kwa ubadhirifu wa zaidi ya Shilingi bilioni 1.9 za ununuzi wa eneo hilo la ekari 29.9 na kulipa fidia kwa wakazi waliokuwepo ili kupisha ujenzi wa kituo hicho kikubwa cha mabasi.
Gambo amekumbushia ujenzi wa kituo hicho kikuu ambacho alisema mchakato wa maamuzi ya ujenzi wa stendi hiyo yamefanywa na halmashauri katika ngazi ya Baraza la Madiwani na kwenye vikao mwaka 2011/12 , lilipendekeza kujenga stendi kwenye maeneo mawili ya Moshono na Olasiti na jiji lilipoingia katika ‘Master Plan’ (Mipango Miji).
Aidha, Serikali imeamua kujenga kituo hicho eneo la bondeni na kuhoji Serikali ina mpango gani ya kuruhusu wananchi wa Moshono na Olasiti kuendeleza eneo hilo na kubadili mpango miji.?
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Festo Dugange alisema ni kweli Serikali kwa dhamira ya kuboresha vitega uchumi jiji la Arusha , wakazi wa Moshono na Olasiti waliahidiwa kufidiwa, lakini hata hivyo serikali imeona eneo la bondeni ni kubwa na lipo sehemu nzuri hivyo panafaa kujenga kitega uchumi.
“Halmashauri ya Jiji la Arusha imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 30 katika eneo la Bondeni City kwa ajili ya ujenzi wa Stendi mpya ya kisasa. Stendi mpya itakayojengwa itazingatia pia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo (Machinga), stendi ya teksi, pikipiki, bajaji, Ofisi za Polisi wa Usalama Barabarani na maeneo ya huduma mbalimbali.” alisema na kuongeza.
“Kazi inayoendelea sasa ni taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya Upembuzi Yakinifu wa mradi. Mradi utajumuishwa kwenye Mradi wa Uboreshaji Miundombinu (Tanzania Cities TransformingInfrastructures and Competitiveness - TACTIC) utakao tekelezwa kwenye Halmashauri 45 za Majiji, Manispaa na Miji nchini ambapo Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia.”

0 Maoni