Na Ahmad Mmow, Lindi.
Serikali imezipongeza taasisi za utafiti wa mazao ya kilimo( TARI) kutokana na tafiti zake kutoa matokeo chanya.
Pongezi hizo zimetolewa leo na waziri mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati wa kikao cha wadau wa korosho ambacho kimefanyika leo mjini Lindi.
Waziri mkuu alisema taasisi hizo licha ya kuonesha juhudi kubwa ya kufanya tafiti, lakini pia tafiti hizo zimekuwa zikitoa matokeo chanya ambayo yanasababisha kiwango cha uzalishaji mazao kuongezeka na kuwa bora.
Waziri mkuu alizitaja baadhi ya taasisi hizo za mazao ya kilimo kuwa ni zile zinazofanya tafiti za mazao ya korosho, mkonge na michikichi. Ikiwamo vituo vya Naliendele na Mlingano.
" TARI inafanya kazi nzuri sana . Vituo vinavyofanya utafiti wa korosho( Naliendele) na mkonge pale Mlingano na ile inayofanya utafiti wa michikichi. Vituo hivyo vinafanya kazi nzuri sana," alisema waziri mkuu wa Majaliwa.
Waziri mkuu pia aliwatoa hofu wakulima juu ya mkanganyiko kuhusu makato ya malipo ya pembejeo kwa wakulima wakorosho watakao kopeshwa pembejeo na serikali.
Waziri mkuu amesema ni jambo ambalo halitawezekana na halitatokea kwa wakulima kukatwa shilingi 110 kwa kilo kilo moja ili kulipa deni la viwatilifu watakavyo kopeshwa.
Amesema wakulima watalipa kulingana na kiasi cha pembejeo watakazokopeshwa na gharama za zitakazotokanana na pembejeo hizo. Ikiwamo usafirishaji.
Kwakuzingatia ukweli huo amewaasa wakulima kutoogopa kuchukua pembejeo hizo. Huku akiwataka viongozi kuwahamasisha wakulima kuchangamkia pembejeo hizo.
Aliweka wazi kwamba tayari tani 21,000 za pembejeo, hasa dawa ya unga( sulpher) zimeshaletwa nchini. Pembejeo ambazo zinakidhi mahitaji ya wakulima wote wa korosho kulingana na takwimu zilizipo. Huku akibainisha kwamba licha ya tani hizo 21,000 lakini pia kuna dawa za maji lita 1,300,000 ambazo zitagawiwa kwa wakulima hao wa korosho.
Aidha waziri mkuu amesisitiza kwamba serikali haitambui uwepo wa unyaufu wa korosho maghalani. Kwahiyo ni marufuku kwa waendesha maghala kukata unyaufu korosho za wanunuzi zilizopo kwenye maghala pindi wanaotaka kuziondoa kutoka kwenye maghalani.
Alisema suala la unyaufu halipo kwa mujibu wa sheria bali likuwa linawaumiza wanunuzi na kuwanufaisha wachache ambao wanakata unyaufu.
Katika kuhakikisha agizo lake linafanyiwa kazi, amewaagiza wakuu wa wilaya kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo kwa kuhakikisha hakuna anayekatwa unyaufu kwenye korosho.
Mbali na hayo kiongozi huyo alisema serikali imeamua korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma zitasafirishwa katika bandari ya Mtwara badala ya barabara.
Amesema uamuzi huo unatokanana ukweli kwamba bandari ya Mtwara imeboreshwa na inaweza kumudu kazi hiyo.
Lakini pia waziri mkuu aliwaeleza na kuwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kwamba waliokuwa wanaidai serikali malipo yanayotokanana kupanda miche ya mikorosho ambayo waligawiwa wakulima watalipwa hivi karibuni. Kwani baada ya kufanya tathimini ya kujua kiasi cha fedha zilizokuwa zinadaiwa, tayari imetenga fedha hizo. Ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia deni hilo lilipwe.
0 Maoni