Moro Wapewa Mkopo Wa Bil 1/- Kumilikisha Viwanja


HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imepata nmkopo wa Sh bil 1.128 kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo la ekari 4,500 maeneo ya Tungi. Mkopo huo kutoka Hazina umepatikana baada ya kumalizika kwa mgogoro kati ya wawekezaji wa Star City wa shamba la mkonge la Tungi na Manispaa na Star City na wananchi.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela alisema hayo hivi karibuni kwenye mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika Ukumbi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu la Morogoro chini ya Meya Pascal Kihanga. Machela alisema, mara baada ya kupatiwa ekari hizo , halmashauri ya Manispaa katika vyanzo vyake vya kawaida ilikuwa haina bajeti ya mpango huo, hivyo iliandika andiko na kuliwasilisha Wizara ya Ardhi , Nyumba na Mendeleo ya Makazi kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais , Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Hazina.


“ Andiko hilo limepita la kupatiwa mkopo wa Sh bilioni 1. 128 , hivyo kwa mujibu wa kisheria na kanuni pamoja na kwamba shughuli zote za Manispaa na Baraza la Madiwani zimekasimiwa na Kamati ya Fedha lakini katika kipengele cha mkopo wenye mamlaka ya kupitisha ni Baraza” alisema Machela.


“ Tumeileta kwenye baraza hili ili muweze kuridhia mkopo huu ili tuweza kupima viwanja mara baada ya kuridhiwa na baraza “ alisema Machela. Alisema katika mpango huo vinatarajia kupatikana viwanja 6,250 kutoka ekari 4,500 ambazo zimerudishwa kwa wananchi na wawekezaji wa Star City eneo la Tungi Estate.


Katika mgawanyo Manispaa itapata asilimia 45 ya viwanja vitakavyozalishwa na asilimia 55 itabaki kwa wananchi wa eneo la Star City. Alisema kwenye mkataba huo , Manispaa ya Morogoro inatakiwa kupanga mji katika eneo hilo la ekari 4,500 na gharama ambazo zitatumika ndiyo inapatikana hiyo asilimia 45 ,na kwamba baadhi ya viwanja ni kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi na miliki pandikizi.

Post a Comment

0 Comments