Mambo 6 muhimu ya kufanya kabla ya kustaafu

  


Kustaafu ni msimu mpya ambao kila mwajiriwa anapaswa kuufahamu na kujiandaa kwa msimu huo vyema.

Kumeshuhudiwa watu wakiishi maisha ya taabu na mahangaiko makubwa baada ya kustaafu. Hili linatokana na kutokujiandaa vyema kabla ya kustaafu.

Kwa kufahamu umuhimu wa kujiandaa vyema kabla ya kustaafu; karibu ufahamu mambo 6 muhimu ya kufanya kabla ya kustaafu.

1. Jiandae kisaikolojia

Kustaafu ni kipindi tofauti sana na kipindi ulichokuwa kwenye ajira. Kipindi hiki utakutana na mtindo mpya wamaisha tofauti na ule uliouzoea.

Ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kwa maswala kama vile kukaa bila kupata mshahara, ofisi, gari la kampuni au taasisi, nyumba ya taasisi au kampuni pamoja na manufaa mengine ya wafanyakazi.

Andaa fikra zako kutambua kuwa wakati wa kufaidi mambo mbalimbali kutokana na kazi yako sasa umefikia mwisho.

2. Weka akiba

Ikiwa kazi yako ndiyo uliyokuwa unaitegemea kama chanzo chako cha kipato, basi tafakari juu ya maisha bila kazi hiyo. Hakikisha unaweka akiba ya kutosha itakayokuwezesha kumudu matumizi yako mbalimbali baada ya kustaafu.

Unaweza kuweka akiba ya pesa au ya vitu ambavyo vinaweza kubadilishwa kuwa pesa kama vile ardhi, mifugo au majengo.

3. Lipa madeni

Kumbuka baada ya kustaafu kiwango chako cha kipato kitapungua; hivyo ni muhimu kulipa madeni kabla ya kustaafu ili usije ukahangaishwa na madeni wakati wa kustaafu.

Ikiwa una mkopo au deni la mtu binafsi, basi hakikisha unafanya juu chini ili ulilipe kabla ya kustaafu.

4. Ondoa matumizi yasiyo ya lazima

Kama nilivyotangulia kueleza kwenye hoja zilizotangulia, baada ya kustaafu kiwango chako cha mapato kitapungua.

Hivyo ni muhimu kutazama upya matumizi yako. Hakikisha matumizi yote ambayo hayana umuhimu au ulazima unayaepuka.

Unaweza kuzingatia haya:

Epuka manunuzi makubwa sana. Ikiwa unapanga kununua vitu kama vile gari, nyumba au kiwanja bada ya kustaafu, tafakari vyema suala hilo.

Epuka huduma ambazo siyo za lazima.

Weka utaratibu mzuri wa kutunza wanaokutegemea. Ikiwa una watoto ambao bado wanasoma au ndugu wanaokutegemea, basi weka mikakati stahiki ya kuwatunza.

5. Tafuta chanzo kingine cha pesa

Kwa kuwa ulikuwa unategemea kazi yako kama chanzo chako cha kipato, ni muhimu sana kutafuta chanzo kingine cha kipato. Usisubiri hadi ustaafu ndipo upate chanzo kingine bali anza kutafuta chanzo hicho kabla hujastaafu.

Nimeshuhudia watu wengi wakianzisha biashara baada ya kustaafu lakini wengi huishia kufilisika kutokana na kukosa uzoefu. Ni muhimu ukaanza mapema ili ujijengee uzoefu.

6. Jiunge kwenye bima ya afya

Mara baada ya kustaafu utahitaji huduma za afya hasa kutokana na matatizo mbalimbali ya uzeeni. Unapokuwa umejiunga na bima ya afya utaweza kupata matibabu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Unaweza pia kuwaunganisha wanafamilia wako ili wasikuwekee mzigo mkubwa wa gharama za matibabu. Kwa kufanya hivi utapunguza gharama za matibabu mara baada ya kustaafu.

Hitimisho

Kwa hakika maandalizi mazuri ya kesho hufanywa leo. Ni muhimu kujiandaa kwa kipindi cha kustaafu mapema ili usihangaike wakati utakapostaafu. Kumbuka baada ya kustaafu hutoweza kufanya kazi kwa nguvu tena kama zamani kwani hata nguvu ya mwili imepungua.

Post a Comment

0 Comments