Vikosi vya usalama vya Ukraine vilisema Jumanne vimefanya mashambulizi katika kanisa la kihistoria la Orthodox mjini Kyiv ili kukabiliana na kinachoshukiwa “ni harakati za uasi zinazofanywa na vikosi maalum vya Russia.”
Shambulizi lilifanyika katika eneo la Pechersk Lavra mjini Kyiv.
Taarifa iliyotolewa na vikosi vya usalama vya Ukraine ilisema shambulizi hilo lililenga kulizuia kanisa hilo kutumiwa kama maficho ya vitendo vya hujuma na makundi ya kijasusi, raia wa kigeni au ghala za silaha.
Kanisa la Orthodox la Russia na Kremlin wamelaani shambulizi hilo.
Ukraine Jumatatu imewasihi wakazi wa mji mkuu na maeneo mengine ya nchi kupunguza matumizi ya umeme wakati ikijaribu kutengeneza njia za umeme zilizoharibiwa na mashambulizi ya Russia wakati Shirika la Afya Duniani likitahadharisha kuwa mamilioni ya Waukraine wanakabiliwa na kipindi cha baridi kali chenye “kutishia maisha yao”.
“Kipindi cha baridi kali kitakuwa ni jinsi ya kuweza kuwa hai,” alisema Hans Kluge, mkurugenzi wa kanda ya Ulaya ya WHO.
Kluge aliwaambia waandishi Jumatatu, “mashambulizi katika miundo mbinu ya afya na nishati yanamaanisha kuwa mamia ya hospitali na vituo vya afya haviwezi kutoa huduma kikamilifu, vikiwa havina mafuta, maji na umeme.”
Pia alionya juu ya changamoto za kipekee za afya kwa nchi hiyo, ikiwemo maambukizi ya upumuaji kama vile COVID-19, homa ya mapafu, flu na hatari zaidi za magonjwa ya diphtheria na surua kwa jamii zilizokuwa hazijapatiwa chanjo ya kutosha.
Katika hotuba yake ya kila usiku Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy aliwasihi wakazi wa Kyiv kubana matumizi ya umeme, na kuwataka wakazi katika maeneo mengine yaliyoathiriwa vibaya nchini kufanya hivyo hivyo, ikiwemo Vinnytsia, Sumy na Odesa.
0 Comments